Kutokana na uzoefu wa utoaji mafunzo, wapo vijana wenye vipaji na ndoto lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za msingi
za kijamii na kiuchumi katika kufikia ndoto zao, ikiwemo kushindwa kumudu gharama za kuhudhuria mafunzo au kuendelea na
masomo. Hawa, hasa ni wale walio kwenye makundi maalum, wanaoishi kwenye mazingira hatarishi, au waliopoteza wazazi au
wadhamini wao wakiwa masomoni. Kwa ajili yao, Chuo kimeanzisha Juhudi Maalum kwa jina la ChangaFursa ili kuwafikia vijana hao
na kuwasaidia kutimiza ndoto zao.
Chuo kinatumia mapato ya ndani kutoka fungu la Uwajibikaji wa Kijamii (CSR) kugharamia juhudi hizo. Hata hivyo, kutokana na wingi
wa mahitaji na uchache wa rasilimali tulizonazo, kama Chuo, tunawaalika wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi zetu.
Mahitaji ya walengwa ni pamoja na chakula, mavazi, malazi, matibabu, ada, fedha za kujikimu, vitabu, vifaa vya kujifunzia, vifaa vya
kiteknolojia, ushauri wa kisaikolojia au msaada wa afya ya akili na kazi za muda mfupi wakati wanasoma. Vitabu, zana/vifaa vya
kujifunzia na vifaa vya kiteknolojia vinaweza kuwa vipya au vilivyotumika.
Jinsi ya Kutuunga Mkono:
a. Udhamini
Unaweza kuchagua mtoto wa kumlipia ada, au kumlipia malazi, au kumlipia chakula na usafiri au kumlipia vyote. Au unaweza
kumchukua mtoto mwenye uhitaji na kuishi naye kwako wakati anasoma ili umgharamie kwa ufanisi. Au unaweza kulipia Chuoni
watoto wengi kwa pamoja au kwa makundi kulingana na vipaumbele vyako.
b. Ushirikiano
Wadau mnaweza kusaidia juhudi hizi kwa kushirikiana na Chuo kutoa huduma kama vile vitabu, zana/vifaa vya Sanaa, vifaa vya
kiteknolojia, mavazi, bima za afya, malazi au vifaa vya malazi, au kujenga hosteli, au mahitaji mengine ya msingi. Au
kuwapa/kuwatafutia wanachuo kazi za muda mfupi wakati wanasoma ili waweze kujigharamia wenyewe.
c. Kuchangia
Hii ni kwa wanaotaka kuchangia kwa mara moja. Mchango wowote unapokelewa, kuheshimiwa na kutambuliwa kwa maandishi.
Mchango unaweza kuwafikia wahitaji kupitia kuuleta Chuoni au kuufuata sisi pale ulipo au kupitia Namba ya Malipo au akaunti
ya benki.
Changia Sasa
Karibu kwa mikono miwili kutuunga mkono katika eneo moja kati ya hayo yaliyoainishwa hapo juu, tunaomba uwasiliane nasi kupitia
changafursa@dararts.ac.tz au +255 715 910 010 ili tukupe mwongozo wa uchangiaji.