Karibu Chuo cha Sanaa Dar es Salaam!
Tunakukaribisha kwa moyo mkunjufu kwenye tovuti rasmi ya Chuo cha Sanaa Dar es Salaam. Hapa ni kitovu cha umahiri katika kutoa mafunzo ya fani mbalimbali za Sanaa za kitamaduni na kisasa, pamoja na kufanya tafiti na kutoa ushauri katika tasnia ya Utamaduni na Sanaa nchini Tanzania. Tovuti hii ni rasilimali muhimu inayotoa taarifa, maarifa, na fursa katika tasnia hiyo.
Tovuti yetu inaonesha maono, malengo, na maadili yetu ya msingi, pamoja na mbinu za kuyafikia. Tumejipanga kuhakikisha kila mteja wetu anapata nafasi ya kutimiza ndoto zake, bila ya kujali tofauti za umri, hali, nafasi, kipato, au elimu. Kwa wale wenye vipaji lakini wanakabiliwa na changamoto za msingi ikiwemo kumudu gharama za masomo, tuna juhudi maalum ya ChangaFursa, ambayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tunazigeuza changamoto zao kuwa fursa kwao.
Kupitia tovuti hii, utapata maelezo ya kozi zetu, sifa za kujiunga, gharama zake, pamoja na taratibu zetu. Aidha, tunaelezea shughuli zetu nyingine nje ya mafunzo ambazo zinatutofautisha. Ingawa tumejitahidi kuhakikisha kuwa kwenye tovuti yetu taarifa zote ni sahihi na za hivi karibuni, lakini kozi, sifa za kujiunga na gharama zake zinaweza kubadilika. Ni vema kutumia Maelekezo ya Kujiunga ya ingizo husika.
Kwa wasanii waliopo sokoni, tunawakaribisha kufaidi fursa za kujiendeleza kitaaluma na kifani, na kujenga ushirikiano wa kuzalisha kizazi kipya cha wasanii, kupitia ushuhuda na uzoefu wao. Kwa wadau wa elimu, Utamaduni, na Sanaa, tunathamini michango yenu katika kukuza vipaji na ujuzi na urithishaji wa Utamaduni kwa vizazi vya sasa na baadaye. Tunawakaribisha kushirikiana nasi katika kuendeleza juhudi hizo kwa pamoja.
Tovuti yetu pia inawasogezea karibu Sera, Mipango na Miongozo ya Serikali yetu ambayo ni misingi wa mafanikio ya sekta ya Utamaduni na Sanaa hapa nchini.
Tunatarajia utapata taarifa na maarifa ya thamani kukidhi matarajio yako ya kuitembelea tovuti. Iwapo hutapata unachotafuta, tafadhali wasiliana nasi kwa msaada zaidi. Tunakukaribisha pia kututembelea Chuoni na kutufuatilia kwenye kurasa zetu za mitandao ya kijamii.
Karibu sana!